Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen.
(Mst) Nicodemus E. Mwangela anatoa salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa ndugu, jamaa na marafiki wa
wafiwa, kufuatia ajali ya gari iliyosababisha vifo 19 ikiwa wanaume ni 15 na
wanawake wanne.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema
kutokana na ajali hiyo iliyotokea usiku eneo la Senjele Wilayani Mbozi
ikihusisha magari matatu yaliyokuwa yakielekea Mbeya kugongana, serikali Mkoani
Songwe imetoa majeneza 19 pamoja na usafiri kwa ajili ya kuhifadhi miili ya
marehemu.
“Rais Magufuli amenituma niwape
pole na ametuelekeza kama Mkoa kusimamia Mamlaka za Usalama barabarani kufanya
uchunguzi na hatua zinazo stahili kuchukuliwa, pia ameelekeza tujipange vizuri
kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani”, amesema Brig. Jen. (Mst)
Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema
chanzo cha ajali hiyo kimetokana na gari la abiria aina ya coaster kugongwa na gari
la mizigo lililokuwa nyuma yake kisha coaster kugonga gari la mizigo lililo
kuwa mbele yake na kupelekea gari la abiria kubanwa katikati ya magari mawili
ya mizigo.
Aidha ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa
wa Songwe, kuweka utaratibu maalumu wa magari kupita kwa kupokezana katika
maeneo yote yenye miteremko mikali, kuwepo ukaguzi wa magari kabla hayajaanza
kushuka au kupanda mlima pamoja na kuweka ulinzi wa maeneo hayo.
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E. Mwangela |
