Wanawake Mkoani Songwe wameaswa kutonyamazia vitendo vya rushwa
ya ngono ili waweze kujikomboa kifikra, kiuchumi na kisiasa katika harakati za
kufikia usawa wa kijinsia kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig Jen. (Mst)
Nicodemus Mwangela katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika
Kimkoa Wilayani Ileje, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema rushwa ya
ngono inapaswa ithibitiwe kwa nguvu zote
“Nawasihi sana wanawake wanaokumbana na udhalilishaji huu wa
kuombwa rushwa ya ngono watoe taarifa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Nchini (TAKUKURU) pia wananchi wengine watoe taarifa mara tu
wanapokutana na matatizo ya rushwa ili taasisi husika ziweze kushughulikia”,
amesema Palingo
Ameongeza kwa kuziagiza halmashauri za Mkoa wa Songwe
kuhakikisha zinaendelea kupiga vita unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, taasisi
zote zinazohusika na mapambano hayo ikiwa ni pamoja na dawati la jinsia
kuwachukulia hatua wote wanaofanya vitendo hivyo.
Palingo ameelekeza kuwa halmashauri ziweke mazingira mazuri ya
masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa na wanawake, kutenga fedha kwaajili ya
kuwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kumiliki viwanda na kutoa mafunzo ya ujasiriamali
kwa wanawake.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake Afisa Maendeleo ya Jamii
Roida Kyomo amesema wanawake wamekuwa wakizalisha kidogo kutokana na ukosefu wa
masoko, elimu na mitaji wakti uwezo wa kuzalisha bidhaa na mazao mengi wanayo.
Kyomo ameongeza kuwa uwepo wa mashauri 442 ya unyanyasaji wa
kijinsia unaonyesha kuwa tatizo hilo bado lipo hivyo ameiomba serikali
kuendelea kuhamasisha jamii kuachana na mila kandamizi kwa wanawake ili muda
unaotumika katika kusuluhisha matatizo hayo utumike katika kuzalisha mali ili
kukuza uchumi.
| Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo akionyesha Bidhaa zinazozalishwa na Kikundi cha wanawake wilayani Ileje. |